Je, Ugonjwa wa Virusi vya Ebola na Ugonjwa wa Virusi vya Marburg ni nini?
Ugonjwa wa Virusi vya Ebola (EVD) na Ugonjwa wa Virusi vya Marburg (MVD) yote ni magonjwa ya nadra na mabaya yanayosababishwa na virusi tofauti. Yanapatikana katika kundi la magonjwa linaloitwa Viral Hemorrhagic Fevers (VHFs).
Ingawa haya ni magonjwa mawili tofauti yanayosababishwa na virusi tofauti, hali ya kuugua yanayoisababisha inafanana. Kwa sababu ya hii, namna ambayo magonjwa haya yanashughulikiwa na watoa huduma wa afya na afya ya umma inafanana.
Je, magonjwa haya yanasambazwa vipi?
Unaweza kupata EVD au MVD ikiwa majimaji ya mwili ya mtu ambaye ni mgonjwa (au ameaga dunia kutokana na) moja ya magonjwa haya yanaingia kwenye macho, pua, kinywa, au kwenye ngozi iliyoathirika.
Majimaji ya mwili ni:
- Damu
- Mate
- Jasho
- Mkojo
- Kinyesi
- Matapishi
- Maziwa ya mama
- Majimaji ya amnioti (kioevu karibu na mtoto anayekua ndani ya mwili)
- Manii
Majimaji bado yanaweza kusababisha ugonjwa hata ikiwa yamekauka.
Watu wanaofanya kazi katika mazingira ya huduma za afya (kama vile wauguzi na madaktari), wanafamilia wa karibu ambao wanawatunza jamaa wagonjwa na watu wanaoshiriki katika shughuli za matanga na mazishi wako kwenye hatari kubwa.
Kuna hatari kidogo sana kwa watu ambao hawajawatunza au wametangamana na mtu ambaye anaugua EVD au MVD.
Je, dalili za magonjwa haya ni gani?
Hakuna dalili inayotokea tu kwa magonjwa haya. Kujihisi mgonjwa kutokana na EVD au MDV kunaweza kujumuisha:
- Homa
- Maumivu ya kichwa ama mwili
- Vipele
- Udhaifu au uchovu
- Vidonda vya koo
- Kuendesha (haja kubwa ya majimaji)
- Kutapika
- Maumivu ya tumbo
- Uvujaji damu au kuvilia damu kusikoelezeka
Je, ni dawa au chanjo za aina gani zinazopatikana?
Hakuna chanjo itakayozuia MVD na hakuna dawa ya kutibu wale walio nayo. Kuna chanjo ya kuzuia aina nyingine za EVD, lakin kuna chanjo inayopatikana tu kwa wafanyakazi wa huduma za afya ambao wana uwezekano wa kufanya kazi na mgonjwa wa EVD. Pia kuna dawa ya kutibu aina nyingine za EVD. Watu wanaougua EVD au MVD bado wanapaswa kutafuta huduma za afya. Uwezekano wa kupona ni bora zaidi ikiwa huduma za matibabu zinaanza mapema.
Je, ikiwa nimesafiri kwenye nchi iliyo na EVD au MVD?
Niko kwenye hatari?
Kuna nchi chache tu ambazo zimekumbwa na mkurukupo wa EVD au MVD. Hata hivyo, hata ukisafiri kwenye nchi hizo, huenda kusiwe na uwezekano wa kupata ugonjwa isipokuwa uyaguse majimaji ya mwili ya mtu ambaye ni mgonjwa au ameaga dunia kutokana na ugonjwa huo. Uko kwenye hatari kubwa ikiwa:
- Unafanya kazi katika mazingira ya huduma za afya (kama vile wauguzi na madaktari)
- Unawatunza wanafamilia wa karibu au jamaa wagonjwa
- Unashiriki katika shughuli za matanga au mazishi
Je, ninaweza kufanya nini ili kuzuia EVD au MVD?
Epuka kuwagusa watu wagonjwa na uepuke kutangamana na damu au majimaji ya mwili kutoka kwa yeyote. Nawa mikono yako mara kwa mara kwa sabuni na maji. Usiguse mili ya wafu wakati wa shughuli za matanga au mazishi.
Je, nifanye nini baada ya safari?
Ikiwa ulisafiri kwenye eneo lililo na mkurupuko wa EVD au MVD, angalia ikiwa una dalili (haswa joto) kwa siku 21 baada ya kuondoka nchi hiyo. Ukianza kujihisi mgonjwa, epuka kutangamana na watu wengine na upigie simu idara yako ya afya (kwa Kiingereza). Ikiwa unatafuta huduma za afya, iambie mara moja kuhusu safari yako.